Sio mbaya kwa marafiki wa karibu au ndugu na jamaa kufahamu kushirikiana
nanyi katika mapenzi yenu kama vile wakati wa sherehe au msiba. Pia sio
mbaya kujuliana hali na kutambulisha mambo ya msingi yanayoendelea
katika mahusiano yako wewe na mpenzi wako. Hata hivyo kuna wakati watu
wengine wa pembeni, wawe majirani, ndugu, wazazi au marafiki wanaweza
kuwa ‘sumu’ ya mahusiano yako, hasa pale unapowategemea sana kutoa
msaada, maoni au maelekezo katika maisha yako ya mapenzi. Makala
hii inaeleza mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano
wa rafiki, ndugu, jamaa, au wazazi kuwa ‘sumu’ ya mapenzi yako.
1. Udhibiti wa taarifa kwa wengine: Kadri
unavyoelezea mahusiano yako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi
watu kutoa maoni, na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza
unavyotakiwa kuishi na mwenza wako. Hivyo basi, chukua muda wa kutosha
kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu maswala yako ya mahusiano kabla
haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine. Ni bora ukasoma
vitabu, na makala mbalimbali, hususani zihusuzo tabia na maisha ya
mahusiano, zitafakari vema ili kuona zinahusiana vipi na unayokumbana
nayo katika mahusianao yako.
2. Upekee wa mambo: Tambua
kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya
tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni
ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie
moja kwa moja katika suluhisho lako. Ukitambua hili, utafanya bidii ya
kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo katika
mahusiano na kutafuta suluhisho kabla ya kutegemea watu wengine.
3. Mwenye maamuzi ni wewe: Ni kweli
kuwa kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wengine, na
zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini, hakikisha kuwa
unatambua kuwa wewe mwenyewe ndio mwenye kubeba lawama ya maamuzi
utakayochukua.
4. Kuwa na subira: Usichukue
maamuziya haraka katika mahusiano hususani uamuzi wa kuamua
kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo uhusiano wako.
Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa haraka unajinyima
nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha hususani madhara yanayoweza
kutokea kwa kuwaeleza wengine, au kama ni tatizo, basi kufikiria njia
sahihi ambazo ungeweza kuzitumia kupata suluhu ya tatizo.
5. Fungua njia za mawasiliano kati yenu: Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani yanayohusu mahusiano yenu kwa watu wengine ni kwakuwa umekosa nafasi
ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za kutosha,
jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka
kuwashirikisha watu wengine.
6. Kuweni peke yenu:
Hata kama hautaki kueleza watu kuhusu mambo yanayoendana na maisha yenu, mazingira unamoishi yanaweza kuchangia watu kutaka kuingilia mahusiano yenu –kwa kutoa maelekezo, ushauri au maoni kuhusu muishivyo wewe na mpenzi wako. Inapobidi hakikisha hamuishi karibu na wazazi wenu, ndugu au rafiki wa karibu. Au haufanyi kazi na mwenzi wako sehemu moja, kwani hiyo itakuwa njia rahisi sana ya watu kuona mnavyoishi. Inapobidi kuwa karibu na watu wengine , hakikisha mnakubaliana wewe na mwenza wako namna bora ya kuendesha mawasiliano kati yenu mbele za watu, ili msiwape nafasi ya wao kumi‘soma’ na kisha kuanza waje waanze kutoa ‘maelekezo’ ya vile wanavyoona mnapaswa kuishi.

No comments:
Post a Comment