Makala hii ni tafakari huru kuhusu mambo ya msingi katika mahusiano. Hapa utapata tafakari ya maana ya maneno na imani ambazo zinatutatiza wengi wetu.
1. Mchanganyiko mkubwa kuhusu maana ya mahusiano, mapenzi na ndoa:
Labda kipengele hiki tuanze kwa kueleza kuwa kunaweza kuwepo ndoa,
lakini yasiwepo mahusiano wala mapenzi. Inaweza kuonekana kama
inachanganya kidogo, lakini ndio ukweli wenyewe. Ndoa
ni namna tuu ambayo wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu
rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano.
Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna ya kutaka
kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea kuvunjika,
basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za ndoa
husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana
mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka
kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua.
Hivyo basi, ndoa haijengi mahusiano wala mapenzi. Kiuhalisi inabidi
kwanza yawepo mahusiano na mapenzi kisha ndio kiapo kifanyike, kwani
kinyume cha hivyo ni kuwa unakula kiapo ‘feki’.
Ndio maana basi, ni muhimu kwa wapenzi kutambua kweli kama
wanahitajiana, kuwa kwenye mahusiano na kutafakari kwa uhuru kama kweli
wanataka kuweka kiapo rasmi cha kuwa pamoja.
Kutumia ndoa kama kinga ya kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni
maamuzi magumu ambayo pengine yanaweza yasilete faida hapo baadae.
2.Mahusiano na ndoa nyingi huyumbishwa na Matarajio yasiyo halisi
Kabla hata ya kuingia katika mahusiano na hatimaye ndoa wengi wetu huwa
na matarajio binafsi ya kimaisha. Matarajio haya yanajumuisha vile
tunavyotaka sie wenyewe kuwa hapo baadae, pamoja na matarajio ya vile
tunavyotaka wenza wetu wawe.
Hata hivyo katika hali halisi tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi
kujibadilisha au kujiweka kwa usahihi vile tunavyotamani kuwa (kwa
sababu kwa kila tunachojaribu kufanya kuwa bora, tunajikuta bado tuna
madhaifu mawili matatu). Pamoja na ukweli huu, tunajikuta tupo na
matarajio ya kuwafanya wenza wetu wawe watu wa aina fulani. Kwakuwa
kiasili binadamu ni kiumbe huru, tunajikuta wenza wetu nao wakiwa ‘busy’
kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya
marafiki, utafutaji wa kazi , kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za
kununua, hata kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.
Matokeo yake ukinzani huu wa matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa
mawazo kati ya wawili nyie, na mwanzo wa vita ya chini kwa chini ya
nguvu ya maamuzi katika mahusiano yenu.
3. Kuweza kumbadili tabia mwenza wako
Mojawapo ya jambo ambalo hufanywa na wengi walio katika mahusiano ni
kuwa na ‘tamaa’ ya kutaka kumbadili tabia fulani mwenza wake. Hata hivyo
‘tamaa’ hii ni sehemu ya yale tunayoyaita matarajio yasiyo halisi,
kwani tabia ya mtu hujengwa na mambo mengi sana, ikijumuisha aina ya
makuzi, aina ya mfumo wa imani mtu anaouamini, aina ya marafiki alio
nao, uwezo wake wa kujiamini katika kubadili tabia kwani wengine
wameshakata tamaa kuwa hawawezi kukata tamaa, na zaidi sana, mabadiliko
ya tabia huhitaji mfumo endelevu na wenye kusoma vema asili ya tabia ili
kuweza kuirekebisha.
Hata hivyo wengi wetu kwenye mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile ‘nitakuacha mie ’, kama
sababu ya kumfanya mtu abadilike kitabia.Udhaifu wetu katika kutambua
asili ya tabia ya mtu husika na mbinu za kisayansi za kubadili tabia
hufanya zoezi la kubadilishana tabia kuwa gumu na pengine
lisilowezakana.
4. Kuvumilia ndio kuonyesha upendo na ndio kudumisha mahusiano
Hii ni aina nyingine ya matarajio ambayo sio halisi kwani kiukweli kila
mtu analo jukumu la kufanya bidii kuwa mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba
‘uzembe’ wa mwingine kwa kisingizio tuu cha kuwa unaonyesha upendo
hususani pale ambapo ni kwa uzembe tuu au kutokujali kwake mwenza husika
amefanya jambo fulani.
Kwa jinsi kasumba hii ilivyo enea sio ajabu kukuta mtu akifanya mambo
mabaya kwa mwenza wake kwa makusudi ili tuu eti apime kama kweli mwenza
wake ni mvumilivu.
Kumbuka hapa hatumaanishi kuwa kusamehe ni kosa. Hapana, kusameheana ni
muhimu, lakini sio kwamba ni muhimu tuu katika mapenzi. Kusameheana ni
jambo la asili, na tunapaswa kusameheana kwa mambo mengi nje hata ya
mahusiano.
Tunachosema ni kuwa kuna kasumba
ya baadhi yetu kuona kuwa wanayo ‘haki’ ya msingi ya kukosea eti tuu
kwakuwa tuu mwenza wake analazimika kusamehe ili kuonyesha kweli anao
upendo wa dhati.
Amini usiamini, kasumba hii ya kutarajia aina ya pekee ya kusamehewa na
kuvumiliwa kwa kisingizio tuu cha kuwa upo kwenye mapenzi na mwenza
wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano yenu kwani mwenzi wako nae
ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha, isitoshe na
yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako
kusamehewa na kuvumiliwa kuna mnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegema
kwako kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka
upendo wako kwake.
5. Uaminifu = Upendo= Kudumu kwa mahusiano
Pamoja na ukweli kuwa mwenza wako anatarajia utakuwa muanifu kwake,
elewa kuwa kuwa mwaminifu pekee katika mahusiano yako sio tiketi ya
kudumu kwa mahusiano yenu kwakuwa watu wanaingia kwenye mahusiano sio
tuu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu mmoja muaminifu bali wana mahitaji
mengine wanayohitaji.
Zungumza na mwenza wako, fanya utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo mengine anayohitaji toka kwako.
Pia msikilize anapokutaka urekebishe mambo kadhaa au ufanye mambo
fulani. Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo yanayompendezesha kwa
kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe unadhani kufanya
hivyo kutampendezesha mhusika.
No comments:
Post a Comment